Matthew 26

Shauri Baya La Kumuua Yesu

(Marko 14:1-2; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)

1 aYesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, 2 b“Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”

3 cBasi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. 4 dWakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. 5 eLakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”

Yesu Anapakwa Mafuta Huko Bethania

(Marko 14:3-9; Yohana 12:1-8)

6 fYesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma, 7naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa; akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

8 gLakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? 9Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”

10 hYesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. 11 iMaskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 12 jAlipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. 13Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

(Marko 14:10-11; Luka 22:3-6)

14 kKisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani 15 lna kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16 mTangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.

Yesu Ala Pasaka Pamoja Na Wanafunzi

(Marko 14:12-21; Luka 22:7-23; Yohana 13:21-30)

17 nSiku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”

18 oAkajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.

20 pIlipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 21 qNao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

23 rYesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. 24 sMwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”

25 tKisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?”

Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

(Marko 14:22-26; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)

26 uWalipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

27 vKisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 wHii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 xLakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

30 yWalipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

(Marko 14:27-31; Luka 22:31-34; Yohana 13:36-38)

31 zKisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

“ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’
32 aa Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

33Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

34 abYesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35 acLakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Yesu Anaomba Gethsemane

(Marko 14:32-42; Luka 22:39-46)

36 adKisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” 37 aeAkamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38 afKisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

39 agAkaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

40 ahKisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 aiKesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”

42 ajAkaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44 akHivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

45 alKisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46 amInukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”

Yesu Akamatwa

(Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yohana 18:3-12)

47 anAlipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49 aoMara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.

50 apYesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”

Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.
51 aqGhafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.

52 arNdipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53 asJe, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 atLakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”

55 auWakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56 avLakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

(Marko 14:53-65; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)

57 awWale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58 axLakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

59 ayViongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. 60 azLakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo
61 bana kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62 bbKisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63 bcLakini Yesu akakaa kimya.

Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo,
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu.”

64 beYesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65 bfNdipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66 bgUamuzi wenu ni gani?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67 bhKisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68 bina kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Petro Amkana Bwana Yesu

(Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)

69 bjWakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwepo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

73 bkBaada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”

74 blNdipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

Papo hapo jogoo akawika.
75 bmNdipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.

Copyright information for SwhNEN